Kufikia mwaka 2050, Afrika itakuwa na mojawapo ya nguvu kazi kubwa zaidi duniani, lakini idadi ya watu pekee haitaamua mustakabali wake. Chunguza jinsi tija, ukuaji wa miji, biashara na mabadiliko ya kidijitali vitakavyounda sura ijayo ya bara.
Kila baada ya miezi michache, kichwa kikuu cha habari hujitokeza kikikadiria kuwa Afrika itafafanua uchumi wa dunia katika miongo ijayo. Sababu zinazotajwa huwa zilezile kila mara: Afrika ina idadi kubwa zaidi ya vijana duniani; miji yake inakua kwa kasi kubwa; teknolojia ya simu inasambaa kwa kasi; na eneo huru la biashara la bara zima linaanza kuchukua sura halisi.
Haya yote ni maendeleo mazuri na yenye kutia moyo. Hata hivyo, mara nyingi huwasilishwa kana kwamba yanaongoza moja kwa moja kwenye ukuaji wa kiuchumi — jambo ambalo si la kweli.
Idadi kubwa ya watu haihakikishii uchumi mkubwa; miji mingi haitengenezi utajiri kiotomatiki; upatikanaji mzuri wa intaneti hautoi ajira bora kiotomatiki; na hata mkataba wa biashara huria hauwezi kubadilisha uchumi iwapo biashara bado zinahangaika kusafirisha bidhaa, kuwekeza kwa ujasiri, au kupata wafanyakazi wenye ujuzi stahiki.
Kuna swali zito zaidi ambalo bado hatujaliuliza na kuwajibika nalo kikamilifu:
Ni nini hasa kinachopaswa kutokea ili uchumi wa Afrika uonekane tofauti kabisa kufikia mwaka 2050?
Ili kujibu swali hili kwa usahihi, tunahitaji kuelewa jinsi mifumo ya uchumi inavyotengeneza thamani. Idadi ya watu, miji, biashara na teknolojia vyote ni muhimu, lakini vina umuhimu kwa sababu vinaathiri kipimo kimoja kikuu cha msingi: tija (productivity).
Wanauchumi hutumia neno hili kueleza ni kiasi gani cha thamani ya kiuchumi kinachozalishwa na kila mfanyakazi. Nchi hazitajiriki baada ya muda kwa sababu tu watu wengi zaidi wanafanya kazi, bali kwa sababu kila mfanyakazi mmoja anaweza kuzalisha bidhaa nyingi zaidi, kutoa huduma bora zaidi, au kutatua matatizo magumu zaidi kuliko hapo awali.
Tukilitazama suala hili kwa mtazamo huu, mazungumzo mengi makubwa kuhusu mustakabali wa Afrika yatapata mwelekeo sahihi zaidi wa kimaendeleo:
Ukuaji wa idadi ya watu unaamua ni watu wangapi wanaoweza kufanya kazi.
Ukuaji wa miji unaunda mahali ambapo wanaishi na kufanyia biashara zao.
Biashara inaathiri ukubwa wa masoko wanayoweza kuyahudumia.
Teknolojia ya kidijitali inabadilisha jinsi wanavyoweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Hakuna hata kimoja kati ya hivi kinachotengeneza utajiri kikiwa peke yake; lakini vinapojumuishwa pamoja, huamua iwapo tija ya taifa, wananchi na vijana itapanda au itashuka. Kufikia mwaka 2050, Afrika itakuwa mojawapo ya maeneo muhimu zaidi ya kiuchumi duniani kwa ukubwa wa nguvu kazi; lakini iwapo itakuwa pia mojawapo ya maeneo yenye tija kubwa zaidi duniani, hilo ni swali tofauti kabisa.
Kuelewa tofauti hiyo ndilo lengo letu kuu leo.
Bara lenye wafanyakazi wengi zaidi kuliko wakati wowote katika historia
Katika sehemu hii
Mabadiliko haya huruhusu mishahara ipande, mapato ya kodi yaongezeke na makampuni yawekeze tena kwa ajili ya ukuaji wa baadaye.
Mwenendo mmoja unaounda mustakabali wa Afrika pia ni mmojawapo wa rahisi zaidi kupimika: idadi ya watu wenye umri wa kufanya kazi barani inatarajiwa kukua kwa kasi kubwa katika miongo michache ijayo. Kulingana na Benki ya Dunia, eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara pekee linatarajiwa kuongeza zaidi ya watu milioni 620 wenye umri wa kufanya kazi kufikia mwaka 2050, ongezeko kubwa zaidi kurekodiwa katika eneo lolote duniani. Wakati nchi nyingi za Ulaya na Asia Mashariki zikijiandaa na idadi kubwa ya wazee na kupungua kwa nguvu kazi, sehemu kubwa ya Afrika itashuhudia kinyume chake. Hili mara nyingi huelezewa kama faida ya kidemografia.
Dhana hii ni rahisi: wakati nchi inapokuwa na sehemu kubwa ya watu wenye umri wa kufanya kazi na sehemu ndogo ya wategemezi, uchumi wake unakuwa na uwezekano na uwezo wa ndani (potential) wa kukua kwa kasi zaidi: watu wengi wanaweza kuingiza vipato, kuzalisha bidhaa na huduma, kulipa kodi na kusaidia uwekezaji.
Hata hivyo, neno muhimu zaidi hapa ni uwezo wa ndani.
Utajiri ndani ya taifa hautengenezwi na ukuaji wa idadi ya watu pekee; unakuwepo pale tu wafanyakazi hao wa ziada wanapopata kazi zenye tija. Hapa ndipo mazungumzo yanapokuwa ya kina zaidi.
Kila mwaka, inakadiriwa kuwa vijana milioni 10 hadi 12 huingia kwenye soko la ajira barani Afrika, lakini ni takriban ajira rasmi milioni tatu tu mpya zenye mishahara zinazozalishwa kote barani. Pengo hili halimaanishi kuwa wafanyakazi waliobaki hawafanyi chochote; wengi wanajipatia riziki katika kilimo, biashara ndogo zisizo rasmi, usafirishaji, ujenzi au biashara ndogo za familia. Shughuli hizi hutoa maisha kwa mamilioni ya watu, lakini mara nyingi huingiza vipato vya chini visivyo na uhakika wala uthabiti ikilinganishwa na ajira rasmi.
Changamoto, kwa hivyo, si kutengeneza ajira tu; ni kutengeneza ajira zinazowaruhusu wafanyakazi kuwa na tija kubwa zaidi kadiri muda unavyopita.
Fikiria nchi mbili zenye idadi sawa ya wafanyakazi: moja ina umeme wa kuaminika, usafiri mzuri, upatikanaji wa mitaji na makampuni yanayowekeza katika mitambo ya kisasa; nyingine inakabiliwa na kukatika kwa umeme, barabara mbovu na uhaba wa mikopo. Hata kama nchi zote mbili zina idadi inayolingana ya watu, nchi ya kwanza hakika itazalisha thamani kubwa zaidi ya kiuchumi kwa sababu kila mfanyakazi ana zana bora na mazingira bora ya kufanyia kazi.
Hii ndiyo sababu wanauchumi huangalia ukuaji kama mchanganyiko wa mambo matatu:
nguvu kazi,
uwekezaji,
na tija.
Nguvu kazi inayoongezeka inapanua uwezo wa uchumi, lakini uwekezaji na tija ndivyo vinavyoamua ni kiasi gani cha uwezo huo kinachotumiwa vizuri ili kuleta faida na maendeleo.
Nguvu kazi inayoongezeka ya Afrika inapaswa kutazamwa kama pembejeo ya kiuchumi (input) badala ya matokeo ya kiuchumi (outcome). Inaongeza uwezo wa bara; lakini iwapo uwezo huo utageuka kuwa vipato vya juu unategemea kila kitu kilichojengwa kuwazunguka wafanyakazi hao: elimu, miundombinu, mikopo, uwekezaji wa kibiashara na ubora wa taasisi za umma.
Muundo wa ajira pia una umuhimu mkubwa:
Kulingana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), takriban asilimia 83 ya ajira kote Afrika zipo katika sekta isiyo rasmi, ikipanda hadi asilimia 85 katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara. Biashara zisizo rasmi zinalinda maisha ya watu pale ajira rasmi zinapokosekana; lakini ni ndogo na hazina uwezo wa kupata mikopo mikubwa au kuwekeza katika kutanuka.
Uchumi unapoendelea, tija hupanda si kwa sababu shughuli zisizo rasmi zinatoweka mara moja, bali kwa sababu wafanyakazi wengi zaidi huhamia kwenye biashara zinazoweza kukua, kuwekeza na kushindana kwa ufanisi zaidi. Mabadiliko haya huruhusu mishahara ipande, mapato ya kodi yaongezeke na makampuni yawekeze tena kwa ajili ya ukuaji wa baadaye.
Tukitazama hivi, tunatambua kuwa nguvu kazi inayokua ya Afrika si hakikisho la mafanikio wala si tatizo la kiuchumi; ni sehemu moja tu ya mlinganyo mpana zaidi. Ukuaji wa watu pekee haubadilishi mengi; kile chenye umuhimu ni iwapo kila mfanyakazi mpya anaweza kuzalisha thamani kubwa zaidi kuliko yule aliyemtangulia.
Wafanyakazi hao wataishi wapi na kwa nini jambo hilo ni muhimu?
Katika sehemu hii
Wanauchumi wanaita jambo hili faida za mkusanyiko (agglomeration effects): watu na biashara wakijumuika pamoja, huwa na tija kubwa zaidi.
Nguvu kazi inayoongezeka inatuambia ni watu wangapi wanaoweza kuchangia uchumi; haituambii ni wapi kazi hiyo itafanyika. Hapo ndipo ukuaji wa miji unapokuwa na umuhimu mkubwa.
Afrika inatarajiwa kuwa na watu wengi zaidi mijini katika miongo ijayo: kulingana na makadirio ya OECD, idadi ya watu mijini barani inaweza kurudufika karibu mara mbili, ikitoka watu milioni 700 leo hadi takriban bilioni 1.4 kufikia mwaka 2050. Kufikia wakati huo, takriban Waafrika sita kati ya kila kumi wanatarajiwa kuishi mijini.
Mabadiliko haya mara nyingi hutajwa kama utabiri wa wazi wa kupaa kwa uchumi wa Afrika. Lakini kama ilivyo kwa idadi ya watu, ukuaji wa miji hauna thamani ukiwa peke yake; umuhimu wake wa kiuchumi upo kwenye kile ambacho miji inakiwezesha.
Watu wakiishi karibu huleta mabadiliko makubwa katika jinsi uchumi unavyofanya kazi:
Mkulima kijijini anaweza kusafiri umbali mrefu kufikia wateja, wazabuni au huduma za benki; lakini biashara jijini inaweza kuwafikia wote watatu ndani ya kilomita chache. Gharama za usafiri zinashuka, biashara zinaweza kuhudumia masoko makubwa zaidi, wafanyakazi wana machaguo mengi ya ajira, na makampuni yanaweza kubobea katika utaalamu maalum kwa sababu kuna wateja wa kutosha.
Wanauchumi wanaita jambo hili faida za mkusanyiko (agglomeration effects): watu na biashara wakijumuika pamoja, huwa na tija kubwa zaidi.
Hii ndiyo sababu nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani zina miji mingi iliyoendelea: miji inakusanya ujuzi, mitaji, miundombinu na mawazo kwa namna ambayo ni ngumu kuipata watu wakiwa wametawanyika vijijini. Manufaa haya yanavuka biashara binafsi:
Jiji lenye mamilioni ya wakazi linaweza kuhalalisha uwekezaji mkubwa katika viwanja vya ndege, bandari, reli za mwendokasi, mitandao ya mkonga na usafiri wa umma kwa sababu kuna watumiaji wa kutosha. Vyuo vikuu, hospitali kubwa, vituo vya utafiti na taasisi za kifedha pia vinakuwa rahisi kujiendesha kukiwa na watu wengi karibu.
Uwekezaji huu hufanya jiji livutie biashara zaidi, na kutengeneza mzunguko ambapo shughuli za kiuchumi zinajiimarisha zenyewe. Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa kila jiji linalokua linakuwa na tija zaidi kiotomatiki.
Ukuaji wa miji unaleta fursa lakini unaleta pia mahitaji makubwa:
Nyumba lazima zilingane na ongezeko la watu; barabara zinahitaji kuhimili magari mengi; mifumo ya maji, umeme na uzoaji taka inahitaji uwekezaji endelevu. Ikiwa miundombinu inakua polepole kuliko idadi ya watu, msongamano unaongezeka, usafiri unakuwa usiotabirika na biashara zinakabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji.
Kwa maneno mengine, miji inaweza kuwa injini za tija au vitovu vya upotevu wa rasilimali; tofauti hiyo mara nyingi inategemea mipango miji na uwekezaji badala ya ukubwa wa idadi ya watu pekee.
Utafiti wa OECD unaonyesha kuwa ardhi ya mijini barani Afrika imekuwa ikitanuka kwa kasi kubwa kuliko idadi ya watu wa mijini: badala ya miji kujengwa juu na kuwa minene, inatanuka kwa upana mkubwa ovyo (urban sprawl). Mfumo huu unafanya iwe ghali sana kuweka barabara, umeme, maji na usafiri wa umma kwa sababu miundombinu inapaswa kufunika maeneo makubwa sana ikihudumia watu wachache.
Kwa biashara, gharama hizi ni halisi: kampuni ya usafirishaji inatumia muda mwingi kumfikia mteja; wenye viwanda wanalipa zaidi kusafirisha bidhaa; wafanyakazi wanatumia saa nyingi kwenye usafiri badala ya kuzalisha; na serikali zinalazimika kusambaza bajeti finyu katika maeneo makubwa badala ya kuboresha huduma katika mitaa iliyopo.
Matokeo yake? Miji inakuwa mikubwa bila kuwa na tija zaidi.
Hii ndiyo sababu ukuaji wa miji haupaswi kupimwa kwa idadi ya watu wanaoishi mijini pekee. Swali muhimu zaidi ni iwapo miji hiyo inarahisisha uzalishaji wa thamani kwa watu na biashara. Swali hili linapaswa pia kubadilisha mtazamo wetu kuhusu ajira:
Miji inapokua, mifumo yake ya kiuchumi inakuwa ya aina mbalimbali: viwanda vinaweza kutanuka, lakini pia sekta kama usafirishaji, fedha, afya, utalii, elimu, uundaji wa programu za kompyuta, huduma za kibiashara na nishati jadidifu. Nchi tofauti zitakuwa na nguvu tofauti kulingana na rasilimali zao na mazingira ya uwekezaji.
Kile ambacho sekta hizi zinashirikiana si bidhaa wanazotengeneza; ni kwamba zote zinategemea wafanyakazi wenye ujuzi sahihi, wafanyabiashara walio tayari kuwekeza, na miundombinu inayoruhusu kufanya kazi kwa ufanisi.
Elimu kwa hivyo inakuwa sehemu ya simulizi ya ukuaji wa miji:
Kuingiza watoto wengi shuleni ni mafanikio makubwa, lakini kuandikishwa pekee hakutoshi; ukuaji wa kiuchumi unategemea kile ambacho wanafunzi wanajifunza na iwapo stadi hizo zinaendana na mahitaji ya viwanda vinavyokua. Nguvu kazi kubwa ya mijini inatengeneza fursa pale tu makampuni yanapoweza kupata wafanyakazi wenye ujuzi wa kiufundi na kitaalamu wanaohitajika.
Kufikia mwaka 2050, miji ya Afrika bila shaka itakuwa mikubwa zaidi kuliko ilivyo leo; iwapo itakuwa vitovu vya uvumbuzi, viwanda na huduma au maeneo ambapo miundombinu inahangaika kuendana na mahitaji, itategemea jinsi ukuaji huo unavyosimamiwa kwa busara.
Idadi ya watu inaongeza wanaoweza kufanya kazi.
Miji inaunda mazingira ambamo kazi hiyo inafanyika.
Swali linalofuata: je, wafanyakazi hao na biashara hizo wataweza kuhudumia masoko yanayovuka miji na nchi zao? Hapo ndipo biashara inapochukua nafasi yake.
Biashara ndani ya Afrika ni zaidi ya kupunguza ushuru wa forodha
Katika sehemu hii
Hivi vinajulikana kama vikwazo visivyo vya kiushuru (non-tariff barriers), na vinaweza kuwa ghali zaidi kuliko ushuru wenyewe.
Miji ya Afrika inapokua, biashara zinapata masoko makubwa ya ndani. Hatua inayofuata ni kurahisisha biashara hizo kuwafikia wateja nje ya mipaka yao. Hilo ndilo lengo kuu la Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Itakapotekelezwa kikamilifu, AfCFTA itaunganisha nchi 54, soko la watu zaidi ya bilioni 1.3 na Pato la Taifa la pamoja la takriban dola trilioni 3.4, na kuifanya kuwa eneo kubwa zaidi la biashara huria duniani kwa idadi ya nchi zinazoshiriki.
Takwimu hizi ni nzuri, lakini hazielezi kwa nini mkataba huu una umuhimu mkubwa wa kiuchumi:
Watu wengi wakisikia "mkataba wa biashara huria" huwaza mara moja kuhusu ushuru wa forodha. Ni dhana ya kawaida kwa sababu kodi za forodha zimekuwa kikwazo kikubwa cha biashara ya kimataifa kihistoria.
Lakini barani Afrika, ushuru wa forodha ni sehemu ndogo tu ya picha nzima; kwa biashara nyingi, changamoto kubwa haijawahi kuwa kodi inayolipwa mpakani, bali kila kitu kinachotokea kabla na baada ya kufika mpakani.
Mzigo unaosafiri kati ya nchi mbili jirani unaweza kukumbana na ucheleweshaji wa siku nyingi mipakani, taratibu tofauti za forodha, viwango tofauti vya ubora, urasimu mwingi wa makaratasi na mifumo ya kisheria isiyotambua ya wengine. Kila ucheleweshaji unapandisha gharama; kila karatasi ya ziada inachukua muda; na kila kutotabirika kunafanya biashara kuwa ngumu.
Hivi vinajulikana kama vikwazo visivyo vya kiushuru (non-tariff barriers), na vinaweza kuwa ghali zaidi kuliko ushuru wenyewe.
Fikiria mtengenezaji wa vyakula vilivyosindikwa nchini Ghana anayetaka kuuza bidhaa zake Côte d'Ivoire, au kampuni ya dawa nchini Kenya inayotaka kuhudumia hospitali nchini Uganda: hata kama ushuru wa forodha ungekuwa sifuri, ucheleweshaji mipakani na sheria zinazogongana hufanya biashara ya kikanda kuwa ya polepole na ghali zaidi kuliko kuagiza bidhaa kutoka nje ya bara!
Hii ndiyo sababu kuu inayofanya biashara ndani ya Afrika kubaki ndogo sana kihistoria ikilinganishwa na maeneo mengine ya dunia.
Kulingana na Benki ya Dunia, faida kubwa zaidi za kiuchumi za AfCFTA zinatarajiwa kutokana si na kupunguza ushuru, bali na kufanya biashara iwe rahisi kiutendaji.
Uchambuzi wake wa mwaka 2020 ulikadiria kuwa utekelezaji kamili wa AfCFTA unaweza kuongeza mapato ya kikanda kwa asilimia 7, sawa na takriban dola bilioni 450 kufikia 2035, huku ukisaidia kuwaondoa watu takriban milioni 30 kutoka kwenye umaskini uliokithiri. Muhimu zaidi, utafiti ulibaini kuwa theluthi mbili ya faida hizo zinazotarajiwa zitatokana na kurahisisha taratibu za biashara — kama forodha za kidijitali na taratibu rahisi — badala ya punguzo la ushuru pekee.
Matokeo hayo yanabadilisha jinsi makubaliano haya yanavyopaswa kueleweka:
AfCFTA haihusu tu kuruhusu bidhaa kuvuka mipaka kwa gharama ndogo; inahusu kuondoa migogoro na vikwazo vinavyozuia biashara kupanuka kote barani.
Kupunguza gharama za biashara kuna manufaa yanayovuka wauzaji wa nje pekee: biashara zinapohudumia masoko makubwa zaidi, zinakuwa na mtaji wa kuwekeza katika mitambo mipya, kuboresha uzalishaji na kuajiri watu wengi zaidi. Masoko makubwa pia yanahimiza ushindani, unaoleta bidhaa bora, bei nafuu na uvumbuzi zaidi.
Kampuni inayohudumia wateja wa jiji moja tu ina ukomo wa kukua; kampuni inayoweza kuwafikia wateja katika nchi kadhaa inaweza kuhalalisha uwekezaji mkubwa zaidi wa viwanda.
Uhusiano huo kati ya ukubwa wa soko na uwekezaji ndio uliojenga uchumi wa nchi nyingi zilizofanikiwa duniani. Na ndiyo maana biashara ni muhimu kwa ajili ya tija: biashara zikiweza kuuza kwa wateja wengi bila vikwazo visivyo vya lazima, zinapanua uzalishaji, zinanunua teknolojia bora na kuajiri wataalamu. Maboresho hayo yanamruhusu kila mfanyakazi kuzalisha thamani kubwa zaidi.
Mikataba ya biashara inaweka sheria, lakini sheria pekee hazisafirishi mizigo kuvuka mipaka; mafanikio yanategemea utekelezaji halisi: forodha lazima ziwe na ufanisi, mamlaka za mipakani zishirikiane, viwango vya ubora vitambuliwe na nchi zote, na miundombinu ya usafiri iendelee kuboreshwa.
Kutia saini mkataba ni mwanzo tu; kipimo halisi cha mafanikio kitakuwa iwapo itakuwa rahisi kwa mjasiriamali wa Kigali kuuza bidhaa zake Lagos, au mtengenezaji wa Misri kupata zana kutoka Kenya, au kampuni ya kiteknolojia ya Nigeria kutanuka kuelekea Kusini mwa Afrika bila vikwazo katika kila hatua.
Biashara haitengenezi thamani kwa sababu tu bidhaa zinavuka mipaka; inatengeneza thamani pale biashara zinapofikia masoko mapana, kuwekeza kwa ujasiri na kuongeza tija kutokana na fursa hizo.
Kanuni hiyohiyo inaeleza jambo lingine linalounda uchumi wa Afrika: katika miongo miwili iliyopita, teknolojia ya kidijitali imepunguza gharama za mawasiliano, malipo na kuendesha biashara. Kama ilivyo kwa biashara, mchango wake mkubwa si teknolojia yenyewe, bali jinsi inavyowaruhusu watu na biashara kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Hapo ndipo uchumi wa kidijitali wa Afrika unapoingia katika picha kamili.
Uchumi wa kidijitali wa Afrika unakua, lakini thamani yake halisi ipo kwingineko
Katika sehemu hii
Fursa halisi ipo kwenye kusaidia biashara katika kila sekta kutumia zana za kidijitali kuwa na tija zaidi.
Mazungumzo kuhusu uchumi wa kidijitali wa Afrika mara nyingi hujikita kwenye kampuni changa za teknolojia (startups), au thamani za mabilioni ya dola. Simulizi hizo ni muhimu, lakini zinaweza kutoa taswira kwamba teknolojia inabadilisha bara ikiwa peke yake.
Ukweli mpana ni wa vitendo zaidi: teknolojia ya kidijitali inatengeneza thamani ya kiuchumi inapofanya shughuli za kila siku za kiuchumi kuwa za haraka, nafuu na za kuaminika zaidi. Biashara inayoweza kupokea malipo papo hapo, kuwasiliana na wazabuni kwa urahisi au kuwafikia wateja mtandaoni inakuwa na tija zaidi, hata kama haijiiti kampuni ya teknolojia kamwe.
Kwa maana hiyo, uchumi wa kidijitali wa Afrika unahusu kile ambacho teknolojia inaziwezesha sekta nyingine kufanya badala ya sekta ya teknolojia yenyewe peke yake. Mfano ulio wazi zaidi ni mawasiliano ya simu.
Kulingana na GSMA, teknolojia na huduma za simu zilichangia takriban dola bilioni 240 kwenye uchumi wa Afrika mwaka 2025, sawa na asilimia 7.8 ya Pato la Taifa la bara. Kufikia 2030, mchango huo unatarajiwa kupanda hadi takriban dola bilioni 290 kadiri simu janja na intaneti zinavyozidi kusambaa. Namba hizi zinawakilisha zaidi ya mapato ya kampuni za simu pekee:
Zinajumuisha shughuli za kiuchumi ambazo simu zinawezesha katika kilimo, biashara, benki, usafiri, afya, elimu na sekta nyingine nyingi. Wakulima wanapata taarifa za bei kabla ya kuuza mazao; wafanyabiashara wadogo wanawasiliana na wateja kupitia programu za ujumbe; madereva wanatumia ramani za kidijitali kupunguza muda wa safari; na wajasiriamali wanatangaza bidhaa mtandaoni bila kuhitaji maduka ya gharama kubwa ya kukodi.
Teknolojia yenyewe ni sehemu tu ya hadithi; mchango wake halisi ni kupunguza muda na gharama zinazohitajika kutekeleza shughuli za kila siku za kiuchumi. Huduma za fedha kupitia simu (mobile money) zinaonyesha hili wazi:
Kabla ya huduma za fedha za kidijitali kuenea, kutuma pesa mara nyingi kulihitaji kusafiri kwenda benki, kutumia njia zisizo rasmi au kusafiri na pesa taslimu umbali mrefu — njia ambazo zilikuwa za polepole, ghali na hatari.
Leo, mamilioni ya Waafrika wanahamisha pesa, kulipa bili, kupokea mishahara na kufanya miamala ya kibiashara kupitia simu zao. Urahisi huu unaweza kuonekana wa kawaida sasa, lakini athari zake za kiuchumi zimekuwa kubwa na zinazopimika:
Utafiti uliochunguza Côte d'Ivoire, Ghana, Kenya, Senegal na Tanzania ulibaini kuwa kufikia mwishoni mwa mwaka 2023, Pato la Taifa katika nchi hizi lilikuwa kati ya asilimia 8 na 10 juu zaidi kuliko ambavyo lingekuwa bila huduma za fedha kupitia simu. Nchini Ghana, watafiti walikadiria kuwa mchango wa huduma za fedha kupitia simu ulikuwa unalingana na pato lote la sekta ya viwanda ya nchi hiyo!
Matokeo haya yanaonyesha kuwa miundombinu ya kidijitali haibadilishi tu jinsi watu wanavyowasiliana; inabadilisha jinsi uchumi unavyofanya kazi.
Mfumo huohuo unaanza kuonekana kwingineko: majukwaa ya kidijitali yanasaidia biashara kupata wateja mbali zaidi; kampuni za usafirishaji zinatumia mifumo ya kidijitali kuboresha njia za usambazaji; serikali zinapanua huduma za kidijitali kwa umma; na kampuni za fintech zinaendelea kupanua upatikanaji wa mikopo. Hata hivyo, hakuna hata moja kati ya haya linaloondoa hitaji la barabara, bandari, umeme au viwanda.
Teknolojia ya kidijitali inakamilisha miundombinu halisi, badala ya kuichukua nafasi yake: duka la mtandaoni bado linategemea barabara kufikisha mizigo; mtengenezaji anayetumia programu za kisasa bado anahitaji umeme wa uhakika kuendesha mitambo; na kampuni inayounda akili mnemba (AI) bado inahitaji wafanyakazi wenye ujuzi, intaneti imara na mitaji.
Miundombinu ya kidijitali inafanya shughuli zilizopo ziwe na ufanisi zaidi; haiondoi misingi ambayo uchumi unajengwa juu yake. Ni muhimu pia kuelewa kwamba mageuzi ya kidijitali ya Afrika bado yanaendelea na hayajakamilika: upatikanaji wa intaneti na stadi za kidijitali bado unatofautiana sana kati ya nchi na nchi na kati ya miji na vijijini. Fursa halisi ipo kwenye kusaidia biashara katika kila sekta kutumia zana za kidijitali kuwa na tija zaidi.
Ukiiweka sambamba na ongezeko la watu, ukuaji wa miji na biashara ya kikanda, uchumi wa kidijitali unakuwa sehemu ya mfumo mpana zaidi:
Nguvu kazi inayoongezeka inapanua idadi ya wanaoweza kuchangia uchumi.
Miji inawaleta wafanyakazi hao karibu na biashara na masoko.
Biashara inapanua idadi ya wateja ambao makampuni yanaweza kuwafikia.
Teknolojia ya kidijitali inasaidia biashara hizo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Kila kimoja kinaimarisha vingine; lakini hakuna kimoja kinachohakikisha vipato vya juu kikiwa peke yake. Vyote vinarudi kwenye swali lilelile la msingi:
"Je, mifumo ya uchumi ya Kiafrika inaweza kumwezesha kila mfanyakazi kuzalisha thamani kubwa zaidi kuliko hapo awali?"
Jibu la swali hili ndilo litakaloamua jinsi uchumi wa Afrika utakavyokuwa ifikapo mwaka 2050.
Afrika inaweza kufananaje kufikia mwaka 2050?
Katika sehemu hii
Hali hii ya tatu huenda ndiyo halisi zaidi: Afrika haitasonga mbele kwa mwelekeo mmoja unaofanana kila mahali.
Mpangilio umeanza kuonekana wazi: ukuaji wa watu, ukuaji wa miji, biashara ya kikanda na teknolojia mara nyingi huzungumziwa kama mambo yaliyojitenga, lakini kiuhalisia yameungana kwa ukaribu sana.
Kuelewa mustakabali wa Afrika kunahitaji kutazama zaidi ya takwimu moja moja: idadi ya watu inaweza kurudufika; miji inaweza kuendelea kutanuka; simu zinaweza kuenea zaidi; na biashara ya kikanda inaweza kuongezeka; lakini hakuna hata moja kati ya haya linaloleta vipato vya juu kiotomatiki. Swali lenye umuhimu ni iwapo yatasababisha tija kubwa zaidi.
Yakifanya hivyo, uchumi wa Afrika mwaka 2050 unaweza kuonekana tofauti kabisa na wa leo; yasipofanya hivyo, changamoto nyingi za kimuundo zitaendelea kuwepo licha ya mabadiliko makubwa ya idadi ya watu na teknolojia.
Badala ya kuwaza mustakabali mmoja usioweza kuepukika, inafaa kufikiria hali tatu tofauti zinazowezekana:
Hali ya Kwanza: Afrika yenye tija kubwa zaidi
Katika hali hii, uwekezaji mwingi wa muda mrefu unaanza kuimarishana: mifumo ya elimu inatoa wahitimu wenye stadi thabiti za kiufundi; biashara zinawekeza kwa ujasiri kwa sababu miundombinu inatabirika na sheria ziko wazi; miji inakua kwa namna inayofanya usafiri na huduma viwe na ufanisi; AfCFTA inashusha gharama za biashara mipakani na kufungua masoko mapana; na teknolojia inashusha gharama za miamala katika kila sekta.
Katika mazingira haya, biashara zinakuwa na tija kubwa zaidi; wafanyakazi wanaweza kuzalisha thamani kubwa kwa sababu wana zana bora, ujuzi wa juu na masoko mapana; ajira rasmi zinanawiri sambamba na ujasiriamali, zikizalisha vipato thabiti na mapato mazuri ya kodi kwa serikali kuwekeza kwenye afya, elimu na miundombinu.
Ongezeko la watu hapa linakuwa faida ya kweli ya kiuchumi, na faida ya kidemografia inaonekana wazi si kwa sababu idadi ya watu iliongezeka, bali kwa sababu kila mfanyakazi wa ziada anachangia zaidi kwenye uchumi kuliko kizazi kilichopita.
Hali ya Pili: Ukuaji bila tija ya kutosha
Hali ya pili pia inawezekana: idadi ya watu inaendelea kukua, miji inazidi kutanuka, simu zinasambaa, na nchi zaidi zinatekeleza AfCFTA; lakini tija inaboreka kwa kasi ndogo sana.
Biashara zinaendelea kukabiliwa na umeme usioaminika, usafirishaji ghali, uhaba wa mikopo na kodi zisizotabirika; shule zinaandikisha wanafunzi wengi lakini viwango vya stadi vinabaki chini; na ukuaji wa miji unazidi miundombinu, ukitengeneza miji mikubwa iliyojaa msongamano usio na tija.
Shughuli za kiuchumi bado zinaongezeka kwa sababu kuna watu wengi zaidi wanaonunua na kuuza; Pato la Taifa linakua, masoko ya walaji yanapanuka, na mahitaji ya nyumba na chakula yanapanda; lakini kipato cha mtu binafsi kinakua polepole sana, polepole kama mwendo wa konokono.
Hii ni tofauti kubwa kwa sababu uchumi unaweza kuwa mkubwa bila kuwa tajiri: nchi yenye watu wengi itazalisha bidhaa nyingi kwa jumla, lakini haimaanishi kila kaya ina maisha bora. Katika hali hii, Afrika inabaki kuwa soko muhimu kwa sababu tu ya ukubwa wa idadi ya watu, lakini ukuaji wa tija unashindwa kufikia uwezo wake.
Hali ya Tatu: Maendeleo yasiyo sawa
Hali hii ya tatu huenda ndiyo halisi zaidi: Afrika haitasonga mbele kwa mwelekeo mmoja unaofanana kila mahali.
Baadhi ya nchi zitapiga hatua kubwa huku nyingine zikienda polepole: miji mikubwa yenye miundombinu imara itavutia uwekezaji na kujenga viwanda vyenye tija kubwa, huku vitovu vingine vya mijini vikihangaika na msongamano na huduma duni; baadhi ya serikali zitatekeleza mageuzi ya kibiashara kwa ufanisi, wakati nyingine zitaendelea kuwa na urasimu; na uvumbuzi wa kidijitali utasambaa kwa kasi katika masoko fulani huku ukibaki mdogo kwingineko.
Hili si jambo la ajabu: maendeleo ya kiuchumi mara chache hutokea kwa usawa duniani; Asia Mashariki, Ulaya na Amerika Kaskazini zote zilipitia vipindi ambapo baadhi ya miji na sekta zilipiga hatua haraka zaidi kabla maendeleo hayajaenea kote.
Uanuwai wa Afrika unaonyesha mtindo kama huo unawezekana: badala ya hadithi moja ya bara zima, kunaweza kuwa na hadithi kadhaa za kitaifa na kikanda zikitokea kwa wakati mmoja: nchi fulani zinaweza kuwa vitovu vya viwanda, nyingine zikabobea kwenye huduma za kidijitali, utalii, usafirishaji, nishati safi, kilimo au huduma za fedha.
Sekta zinaweza kuwa tofauti, lakini kanuni kuu haibadiliki: nchi zinazoboresha tija mara kwa mara zina uwezekano mkubwa wa kushuhudia maisha ya wananchi wake yakipanda kuliko zile zinazotegemea ongezeko la watu pekee.
Uzi mkuu unaounganisha yote
Kutazama hali hizi tofauti kunaleta hitimisho moja thabiti: sehemu inayotabirika zaidi ya mustakabali wa Afrika si kiwango cha mapato yake, bali ni idadi na umri wa watu wake.
Makadirio ya idadi ya watu yanaweza kubadilika kidogo, lakini mwelekeo mkuu uko wazi: bara litakuwa na watu wengi zaidi wa umri wa kufanya kazi katika miongo ijayo kuliko lilivyo nayo leo.
Kila kitu kingine kiko mikononi mwa maamuzi:
Ubora wa elimu unaweza kuboreka au kudumaa.
Miundombinu inaweza kwenda sambamba na ukuaji wa miji au kubaki nyuma.
Biashara zinaweza kuchagua kuwekeza au kuahirisha upanuzi.
Mikataba ya biashara inaweza kutekelezwa kikamilifu au kubaki kwenye makaratasi.
Teknolojia inaweza kuenea katika uchumi mzima au kubaki katika sekta chache.
Haya ni maamuzi ya kiuchumi, si matokeo ya moja kwa moja ya kidemografia. Hiyo ndiyo sababu mijadala kuhusu mustakabali wa Afrika inapaswa kujikita zaidi kwenye kujenga mazingira yanayoiwezesha idadi hiyo kuwa na tija kubwa badala ya kuangalia ukubwa wa namba pekee.
Hitimisho
Katika sehemu hii
Ongezeko la watu linafanya uwekezaji huu wote uwe wa dharura na muhimu zaidi; halichukui nafasi yake.
Sura ijayo ya kiuchumi ya Afrika haitaandikwa na idadi ya watu pekee.
Nguvu kazi kubwa inatengeneza fursa, lakini fursa si sawa na utajiri. Utajiri hujitokeza wakati wafanyakazi wana ujuzi wa kutatua matatizo magumu, biashara zina ujasiri wa kuwekeza, miji inasaidia shughuli za kiuchumi badala ya kuzikwamisha, masoko yanafikika kwa urahisi, na taasisi zinatengeneza mazingira ambapo tija inaweza kuendelea kukua siku baada ya siku.
Ongezeko la watu linafanya uwekezaji huu wote uwe wa dharura na muhimu zaidi; halichukui nafasi yake.
Kufikia mwaka 2050, Afrika hakika itakuwa nyumbani kwa mojawapo ya nguvu kazi kubwa zaidi duniani. Hilo tayari linaonekana katika makadirio ya idadi ya watu.
Iwapo itakuwa pia mojawapo ya maeneo yenye tija kubwa zaidi duniani inategemea maamuzi yanayofanywa leo na serikali, wafanyabiashara, wawekezaji, walimu na wajasiriamali kote barani humu.
Mustakabali, kwa maneno mengine, hauamuliwi na idadi ya watu ambao Afrika itakuwa nao; unaamuliwa na kile ambacho watu hao wataweza kukijenga na kukizalisha.
Hii ndiyo makala ya mwisho katika mfululizo wetu wa: Jinsi Afrika Inavyotengeneza Thamani ya Kiuchumi. Ikiwa umefurahia makala hii, jiunge na jarida letu; kwa pamoja tunaweza kuchangia ukuaji wa Afrika kupitia biashara na utalii. Unaweza pia kushiriki makala hii na rafiki.
Marejeleo
Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) (2021). Mkataba wa Kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika.https://au-afcfta.org/
Umoja wa Mataifa, Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, Kitengo cha Idadi ya Watu (2024). Matarajio ya Idadi ya Watu Duniani 2024.https://population.un.org/wpp/
Benki ya Dunia (2020). Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika: Athari za Kiuchumi na Mgawanyo. Washington, DC: Benki ya Dunia. https://doi.org/10.1596/978-1-4648-1559-1